SERIKALI imesema itakamilisha ujenzi wa shule za Sekondari
1,200 kwa kuweka miundombinu muhimu ikiwemo umeme kupitia Mpango wa Maendeleo
wa Elimu ya Sekondari awamu ya pili.
Kauli hiyo imetolewa leo Bungeni mjini Dodoma na Naibu
Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa, Mhe. Majaliwa Kassim Majaliwa wakati
akijibu swali la Mbunge wa Dodoma Mjini, Mhe. Dk. David Mallole, aliyetaka kujua Serikali ina mpango
gani wa kupeleka umeme kwenye Shule za Kata hasa za Bweni.
Mhe.Majaliwa amesema kuwa kwa awamu ya kwanza Serikali
imeanza kukamilisha ujenzi kwa shule 264 kwa thamani ya shilingi Bilioni 56.3
ambapo suala la umeme wa gridi ya taifa na umeme wa jua limepewa kipaumbele.
Ameongeza kuwa Serikali kupitia mfuko wa wakala wa usambazaji
umeme Vijijini (REA) imedhamiria kusambaza umeme katika zahanati, shule na
visima vya maji vilivyo katika maeneo yatakayonufaika na huduma hii ya umeme
Vijijini.
“Mpaka sasa, Serikali imewezesha shule za sekondari 3,385
sawa na asilimia 75 ya shule zote za sekondari nchini kuwa na huduma ya umeme”
amesema Mhe. Majaliwa.
Ameongeza kuwa Serikali itaendelea kishirikiana na wadau na
kupitia miradi mbalimbali ya maendeleo kuhakikisha dhamira ya kuziwezesha shule
na maeneo mengine yanayotoa huduma za jamii yanakuwa na huduma ya uhakika ya
umeme.
EmoticonEmoticon