MATOKEO MABAYA KIDATO CHA NNE 2012, VYUO VYA UALIMU KUKOSA WANAFUNZI ELFU 50,000

Athari za Matokeo ya Kidato cha IV 2012: 
 
vyuo vingi kukosa wanafunzi wakudahili, kwa asilimia 50%,
huku Dira ya maendeleo ya taifa ya 2025 ikuyumba.

Reported by Dr Kitila Mkumbo
Senior Lecturer in Psychology and Education
Dean, Faculty of Education Dar es salaam University (DUCE)

Kama ilivyotarajiwa, idadi kubwa ya wanafunzi waliofanya mtihani wa kidato cha nne mwaka jana wamefeli. Kati ya wanafunzi 367,750 waliofanya mtihani na ambao matokeo yao hayakuwa na kuzuizi, wanafunzi 240,903 wamefeli kwa kupata daraja la 0 (Tazama umbo Na.1). Hii ni sawa na asilimia 65.5 ya wanafunzi wote waliofanya mtihani wa kidato cha nne.


Aidha wanafunzi 103,327 ‘wamefaulu’ kwa kiwango cha daraja la nne, ambao ni sawa na asilimia 28.1 (Tazama Umbo Na. 2). Kitaaluma, hawa nao wamefeli kwa sababu kwa mfumo wa elimu wa Tanzania kwa sasa ngazi nyingi za elimu baada ya kidato cha nne kinahitaji ufaulu wa kiwango cha chini cha daraja la tatu. Kwa hivyo ukijumlisha idadi ya wanafunzi waliopata daraja la IV na 0 unapata wanafu
 
344,230 waliofeli kwa kiwango cha daraja la IV na 0; idadi hii ni sawa na asilimia 94 (Tazama Umbo Na. 2)!! Kwa hiyo ni asimia sita (6) pekee ya wanafunzi waliopata madaraja ya I, II na III na ambao kimsingi ndio wenye sifa za kujiunga na ngazi mbalimbali za elimu baada ya kidato cha nne.

Pamoja na kwamba watu wengi wameonekana kushtushwa na matokeo haya, akiwemo waziri mwenye dhamana ya elimu nchini, kwa wataalamu na wafuatiliaji makini wa mambo ya elimu matokeo haya hayashangazi. Tatizo moja la sisi

watanzania tumekuwa ni watu wa kusubiri matokeo na kutokujali sana mchakato unaoletekeza matokeo hayo. Sote tunajua kwamba hizi shule zinazoitwa shule za sekondari kimsingi nyingi zao hazina hata sifa ya shule nzuri ya shule ya msingi.

Utafiti wa karibuni unaonyesha kwamba ni asilimia nne tu ya shule zote za sekondari nchini ndio zenye kukidhi vigezo vya chini kabisa vya shule ya sekondari. Sote tunatambua kuwa walimu siku hizi hawana moyo wa kufundisha baada ya kupuuzwa na kudharauliwa kwa muda mrefu. Walipojaribu kugoma mwaka jana wakatishwa na kusimangwa na mwajiri wao.

Wakarudi madarasani wakiwa wamenuna na wakatuwaaambia waziwazi kwamba ‘mtaona’. Baadhi ya walimu wakadiriki hata kusema kwamba watafundisha madudu na mwalimu mmojawapo akatoa mfano ubaoni kuwa watafundisha ‘7+7=77’. Badala ya kuungana na walimu kuibana serikali sote tukanywea, na mitihani ilipokaribia tukaenda madhahabuni kumuomba Mungu ili watoto wetu wafaulu mitihani yao.

 Matokeo ya mwaka huu ni mabaya zaidi kutokea tangu nchi yetu ianze kuwa na mfumo wa elimu wa kidato cha nne. Haijawahi kutokea hata mwaka mmoja wanafunzi wa kidato cha nne wakafeli kwa kiwango hiki. Kiwango kibaya cha kufaulu kilikuwa mwaka 2010 ambapo asilimia 50.4 tu ya wanafunzi waliofanya mtihani wa kidato cha nne ndio waliofaulu, wakati asilimia 49.6 walifeli (Tazama umbo Na. 3). Ukichunguza kwa makini utaona kwamba kiwango cha kufaulu kilianza kushuka zaidi baada ya wanafunzi waliopitia mfumo wa shule za sekondari za kata walipoanza kumaliza, hasa kuanzia mwaka 2010, tulipoanza rasmi kutekeleza sera ya ‘wingi kwanza ubora baadaye’.

ADHARI ZA MUDA MREFU NA MFUPI

Matokeo haya, kama yalivyokuwa ya miaka ya nyuma, yana athari nyingi, za muda mfupi na muda mrefu ujao. Kwa muda mrefu ujao, matokeo haya yanafifisha azima ya taifa ya kuwa na taifa la watu walioelimika ifikapo mwaka 2025 kama ilivyoanishwa kwenye Dira ya Maendeleo ya Taifa ya 2025.

Kwa matokeo haya na mengine ya miaka mitatu iliyopita, mfumo wetu wa elimu ya sekondari (na hata msingi) unatutengenezea taifa la watu mbumbumbu ambao itakuwa vigumu kuwafanya waamini katika sayansi, achalia mbali wao wenyewe kuibuka kuwa wana sayansi.
  
Lakini pengine athari ambazo zitaanza kuonekana sasa hivi ni shule na vyuo kuanza kukosa wanafunzi wa kudahili. Kwa mfano, idadi ya wanafunzi wanaohitajika kujiunga na mafunzo ya ualimu ngazi ya cheti na kidato cha tano kwa mwaka huu ni zaidi ya 50,000, lakini ni wanafunzi 23,520 tu waliomaiza mwaka jana ndio wenye sifa za kujiunga na taasisi hizi za elimu. 

Hivyo kutakuwa na upungufu wa wanafunzi zaidi ya asilimia 50 wa kujiunga katika vyuo vya ualimu ngazi ya cheti na kidato cha tano ukizingatia kwamba sifa ya chini ya kujiunga na ngazi hizi za elimu ni kidato cha nne na ufaulu wa kiwango cha daraja la tatu. 

Ni wanafunzi hawa waliomaliza mwaka jana wanaotarajiwa kujiunga na vyuo vya elimu ya juu ifikapo mwaka 2015. Kwa upande wa vyuo vikuu pekee, kutakuwa na nafasi zisizopungua 27068 mwaka 2015. 

Hata kama wanafunzi wote waliofaulu kwa kiwango cha daraja la I-III wataenda kidato cha tano na wote hawa wakafaulu mtihani wa kidato cha sita mwaka 2015, bado hawataweza kujaza nafasi za vyuo vikuu zitakazokuwepo mwaka 2015. (tazama maumbo Na. 4 na 5).

Hata hivyo, kwa maoni yangu, hatari kubwa inayotukabiri sio ubaya wa matokeo haya. Hatari kubwa ni kutokujali kwetu. Tena katika hili la elimu ndio kabisa litapita upesi kwa sababu wengi tunaopiga hizi kelele watoto wetu ni miongoni mwa hao asilimia mbili waliopata madaraja ya I na II na ambao wanahudhuria mfumo tofauti kabisa wa elimu! Tutapiga vikelele kidogo kisha tutanyamaza tukisubiri matokeo mengine pengine mabaya zaidi mwakani tusipochukua hatua yeyote ya maana. 

Na hatua ya kwanza ya maana kabisa na ya muda mfupi ni kuwajali walimu. Katika bajeti ijayo serikali iwaongezee walimu mishahara angalau mara mbili ya wanaopata sasa hivi. Tukichukua hatua hii tutaanza kuanza matokeo tofauti. Nimesema mara zote na narudia tena leo kwamba elimu bora ni walimu bora. Hatua za muda mrefu ni kuuangalia upya mfumo wetu wa elimu. Hili litahitaji wataalamu wa elimu waweke vichwa vyao chini. Lakini hili haliwezekani kama serikali yetu itaendelea na sera yake ya ‘wingi kwanza, ubora baadaye’!


Mwandishi wa Makala haya ni Mhadhiri Mwandamizi katika Elimu na Saikolojia
na Mkuu wa Kitivo cha Elimu katika Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu Dar es
Salaam (DUCE).


EmoticonEmoticon