MNYIKA AMJIBU MGIMWA TOZO ZA SIMU, APINGA KUSEMA WABUNGE WALIPITISHA

Alia na wananchi kuongezwa mzigo mkubwa wa kodi, na kutoa hatua 7 ambazo amemtaka waziri wa fedha kutolea ufafanuzi huku akieleza jinsi anavyo hamasisha wananchi kupinga tozo hizo

   > Ataka maandamano,
   > Sahihi ya wananchi wanao pinga kupandishwa kwa tozo hizo,
   > Wabunge waliopitisha sheria hiyo watajwe,
   > Wananchi wapewe taarifa kamili ilikuwaje sheria hiyo ikapitishwa.

Habari kamili

KAULI YA WAZIRI WA FEDHA KUHUSU KODI YA LINE ZA SIMU NI KIELELEZO CHA UDHAIFU WA SERIKALI NA UZEMBE WA BUNGE; NIANDIKIE SASA KUHUSU HATUA ZA KUCHUKUA JUU YA SUALA HILI KUPUNGUZA MZIGO WA GHARAMA ZA MAISHA KWA WANANCHI

Katika kipindi cha Hot Mix cha EATV muda mfupi uliopita Waziri wa Fedha amesema kwamba mawazo ya kutoza elfu moja kwa mwezi kwenye kila laini ya simu ni ya wabunge. 

Kauli inayokaribiana na hiyo imewahi kuandikwa pia na Naibu Waziri wa Wizara yenye dhamana na sekta mawasiliano kwenye mitandao ya kijamii katika siku za karibuni. Baadaye alifuata Naibu Waziri wa Wizara ya Fedha na sasa waziri mwenyewe. Mwaka 2012 nilitahadharisha kuhusu udhaifu wa Rais (na Serikali) na uzembe wa Bunge katika masuala yanayohusu maandalizi ya bajeti, hususan kutozingatiwa kwa mpango wa taifa wa maendeleo na ongezeko la mara kwa mara la gharama za maisha kwa wananchi. Kwa kauli hizi za Serikali udhaifu na uzembe huo unaendelea kujihidhirisha.

Kauli hizi za Serikali ni za kujivua mzigo wa lawama baada ya malalamiko ya wananchi kuhusu kodi hii na nyinginezo kwa kuhamisha mzigo huo kwa wabunge.

Ni muhimu badala ya kutoa kauli za ujumla za kulaumu wabunge, Serikali ijitokeze itaje kwa majina na wabunge gani hasa walitoa mawazo hayo. Mimi sijawahi kutoa wazo hilo wala kuliridhia. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni kwenye Hotuba yake juu ya Muswada wa Sheria ya Fedha ilipinga pendekezo hilo lililokuwepo katika jedwali la marekebisho lililowasilishwa na Wizara ya Fedha. Katika kuhakikisha kwamba kifungu hicho hakipitishwi, niliwasilisha jedwali la marekebisho ya sheria kutaka kifungu hicho kiondolewe katika muswada wa sheria ya fedha na marekebisho yake yaliyowasilishwa na Serikali.

Hata kama ikiwa ni ukweli kwamba wazo hilo ni la baadhi ya Wabunge (ambao ni muhimu wakatajwa kwa majina), Serikali inayokwepa kutetea maamuzi ambayo Serikali yenyewe imeyaunga mkono inadhihirisha kwamba imechoka na imepoteza uhalali kwa kimaadili kwa kushindwa kukubalika mbele ya wananchi wake yenyewe (illegitimate government) . 

Mamlaka na madaraka ya Bunge kwa mujibu wa katiba ibara ya 63 ni kuishauri na kuisimamia Serikali. Katika kutekeleza mamlaka hayo, Bunge ni chombo cha uwakilishi wa wananchi na chenye mamlaka pia ya kutunga sheria na kupitisha bajeti ya nchi. Hata hivyo, ibara ya 99 ya Katiba imeweka mipaka kwa mamlaka hayo ya Bunge inapokuja suala la kutunga sheria ya fedha kama hii iliyoongeza mzigo wa kodi kwa wananchi. Mamlaka hayo yamewekwa kwa kiwango kikubwa mikononi mwa Rais kupitia Waziri wake mwenye dhamana.

SOMA ZAIDI HAPA

KAULI YA WAZIRI WA FEDHA MHE. WILLIUM MGIMWA AMBAYO ANAPINGWA NA MNIKA


EmoticonEmoticon