UTAFITI WA KUPIMA UMAHIRI WA WATOTO KATIKA KUSOMA NA KUANDIKA WAJA

Watafiti wa kujitolea elfu nane kutathmini watoto Tanzania Bara
Utafiti umelenga kupima umahiri wa watoto katika stadi za kusoma na kuhesabu

21 Agosti 2013, Dar es Salaam: Jumla ya watafiti wa kujitolea 7,980 wanashiriki katika Tathmini ya Uwezo katika wilaya 133 za Tanzania Bara. Utafiti huu unalenga kujua uwezo wa watoto katika kusoma Kiswahili, Kiingereza na kufanya hesabu. Tathmini hii ni jitahada za Uwezo kila mwaka kukagua ubora wa msingi wa elimu kwa watoto.

Uwezo inaamini kuwa msingi wa elimu bora kwa watoto unapatikana kwa watoto kujifunza kwa kiwango na ubora unaotakiwa. Lakini, pamoja na jitihada za Serikali na wadau wengine kuboresha miundombinu na vifaa shuleni pamoja na kuajiri walimu, swali la msingi la kujiuliza ni: Je, watoto wetu wanajifunza?

Tathmini ya Uwezo ni zoezi la kisayansi la nchi nzima linalolenga kukusanya takwimu ili kujua stadi na kiwango cha watoto wetu katika kusoma na kufanya hesabu. Utafiti huu unatathmini watoto kwa kiwango cha mtaala wa darasa la pili. Zaidi ya watoto laki moja na hamsini na tano (155,000) wenye umri wa miaka 7 – 16 watatathminiwa mwaka huu. Watoto hawa wanatoka katika kaya 79,000 zilizomo katika vijiji na mitaa 4,000 nchi nzima.

Sababu ya msingi ya kufanya tathmini hii majumbani ni kutoa fursa kwa wazazi kupata matokeo papo hapo ya tathmini kwa watoto wao ili kujua udhaifu upo wapi na wanawezaje kuwasaidia watoto wao. Katika jamii nyingi zilizofanyiwa utafiti, wazazi wamepata mwamko wa kufuatilia na kusaidia watoto masuala yanayohusu elimu ya watoto wao.

Msingi wa mafanikio bora katika elimu upo katika ngazi ya chini kabisa ya kusoma na kufanya hesabu kwa watoto. Uwezo inaamini - kwamba kushindwa kwa watahiniwa wengi wa sekondari katika ngazi ya Kidato cha Nne kunachangiwa, kwa kiasi fulani, na kukosekana kwa stadi muhimu za kusoma na kufanya hesabu kwa watoto. Hii inasababisha hali ya kufeli kujirudia kadiri watoto wanavyosonga mbele katika elimu ya msingi na sekondari.

Katika utafiti wa mwaka jana, Uwezo iliegundua kuwa ni mtoto 1 tu kati ya watoto 5 wa darasa la tatu 3 anayeweza kusoma na kufanya hesabu kwa kiwango cha darasa la 2.

Uwezo inashirikiana na taasisi mbalimbali katika maandalizi na utekelezaji wa tathmini hii ya watoto. Mchakato wa kuchagua sampuli yenye kaya na jamii zinazolengwa wakati wa kukusanya taarifa hufanywa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS). Vifaa vinavyotumika kutathmini watoto hutengenezwa kwa ushirikiano na wataalamu wa vyuo vikuu na Taasisi ya Elimu nchini (TIE). 


Tume ya Sayansi na Teknolojia nchini (COSTECH) hutoa muongozo wa utekelezaji wa utafiti huo. Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi  pamoja na Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) hutoa ushirikiano wao kwa njia mbali mbali ukiwemo ushauri wa ziara kwenye vijiji, mashule na majumbani.

Katika kutekeleza Tathmini hii, Uwezo Tanzania inashirikiana na waratibu wa mikoa 24 wanaosimamia zoezi kupitia kwa waratibu wa wilaya 133 wanaotoka katika asasi zilizopo wilayani mwao. Asasi hizi ni wadau wa maendeleo ya elimu katika wilaya husika. Wasimamizi wa kila wilayani huratibu watafiti wa kujitolea 60 katika zoezi la kukusanya taarifa kwa kushirikiana na viongozi wa serikali za mitaa, walimu na wazazi.

“Nashiriki katika tathmini hii kwa hamasa kubwa kwa sababu naamini kuwa suala la matokeo ya kujifunza kwa watoto ni ajenda muhimu sana katika maendelo ya sekta ya elimu nchini. Tunahitaji kubadili mwelekeo, badala ya kukazana na miundombinu na vifaa pekee, tuhusishe mashirikiano ya wazazi, walimu, viongozi wa serikali za mitaa na wadau wengine katika kuleta mabadiliko chanya” anasema Mathew Chungu, Mratibu wa Uwezo wa Wilaya ya Kibaha Mjini.

“Ni muhimu sana kwa Uwezo kushirikiana na wadau mbalimbali katika ngazi ya mkoa, wilaya na jamii kwa ujumla. Na pia kwa sababu utafiti huu unahusu jamii, Uwezo inaweka mkazo kwenye utoaji wa matokeo ya utafiti kwa jamii kwa njia mbalimbali. Lengo letu ni kuboresha mijadala na kuwezesha wazazi, walimu, taasisi na wadau wengine kushiriki katika jitihada za kuboresha elimu kwa watoto nchini,” anaongeza Zaida Mgalla, Mratibu wa Uwezo Tanzania.

Utafiti huu unatarajiwa kukamilika mwezi Septemba mwaka huu na matokeo yake kutolewa mapema mwakani.


EmoticonEmoticon