Release No. 142
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Agosti 27, 2013
Sekretarieti ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) inaendelea na maandalizi ya Mkutano Mkuu wa Uchaguzi utakaofanyika Oktoba 26 na 27 mwaka huu jijini Dar es Salaam.
Awali mkutano wa uchaguzi ulikuwa ufanyike Februari 23 na 24 mwaka huu lakini tukauahirisha kusubiri maelekezo ya Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA), hivyo tayari wajumbe wana taarifa rasmi kuhusu mkutano huo.
Orodha ya wajumbe iliyotumwa awali kwa ajili ya Mkutano tunayo, isipokuwa kama kuna wanachama wetu wana mabadiliko ya majina ya wajumbe watakaohudhuria wanatakiwa kutuma majina hayo kabla ya Septemba 30 mwaka huu.
Wanachama wa TFF ni vyama vya mpira wa miguu vya mikoa, vyama shiriki na klabu 14 za Ligi Kuu ya Vodacom.
WAWILI WAPINGWA UCHAGUZI WA TFF
Wanamichezo wawili walioomba kuwania uongozi kwenye uchaguzi wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) utakaofanyika Oktoba 27 mwaka huu wamewekewa pingamizi.
Waliopingwa ni Wallace John Karia anayeomba kupitishwa kuwania urais na Vedastus Kalwizira Lufano anayewania ujumbe wa Kamati ya Utendaji kupitia Kanda Namba Mbili ambayo ni mikoa ya Mara na Mwanza. Anyempinga Karia ni Shamsi Rashid Kazumari wa Dar es Salaam wakati Lufano anapingwa wa Samwel Nyalla wa Mwanza.
Pamoja na mambo mengine, Kazumari anampinga Karia kwa madai kuwa akiwa Mwenyekiti wa Kamati ya Ligi, aliwashawishi wajumbe wenzake kuingia mkataba na Azam Tv wakati akijua kamati hiyo ni ya muda, hivyo haina nguvu za kisheria kusaini mkataba huo.
Naye Nyalla ambaye pia ni mmoja wa wanamichezo waliojitokeza kuwania ujumbe kupitia Kanda hiyo anampinga Lufano kwa madai hana uzoefu wa miaka mitano katika uongozi wa mpira wa miguu.
Kamati ya Uchaguzi ya TFF chini ya Mwenyekiti wake Hamidu Mbezeleni itakutana kesho (Agosti 28 mwaka huu) saa 4 kamili asubuhi kusikiliza pingamizi hizo ambapo wawekaji pingamizi na waliopingwa wanatakiwa kufika wenyewe ndani ya muda kwa vile uwakilishi hautakiwi.
YANGA, COASTAL UNION KUUMANA VPL
Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) inaingia raundi ya pili kesho (Agosti 24 mwaka huu) kwa timu zote 14 kuwa viwanjani huku macho na masikio ya washabiki wengi yakielekezwa kwenye mechi kati ya Yanga na Coastal Union.
Mechi hiyo itachezwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kuanzia saa 10.30 jioni kwa kiingilio cha sh. 5,000, sh. 8,000, sh. 15,000 na sh. 20,000. Mwamuzi Martin Saanya wa Morogoro ndiye atakayepuliza filimbi wakati Kamishna atakuwa Omari Walii kutoka Arusha.
Mtibwa Sugar itaikaribisha Kagera Sugar kwenye Uwanja wa Manungu ulioko Turiani mkoani Morogoro wakati Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi mjini Tabora utakuwa mwenyeji wa pambano kati ya wenyeji Rhino Rangers na Azam.
Vumbi lingine litatimka kwenye Uwanja wa Mabatini ulioko Mlandizi mkoani Pwani wakati maafande wa JKT Ruvu watakapokwaruzana na wenzao wa Tanzania Prisons kutoka Mbeya. Mbeya City na Ruvu Shooting zitacheza kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine jijini Mbeya.
Jiji la Tanga litakuwa mwenyeji wa mechi kati ya Mgambo Shooting na Ashanti United itakayochezwa kwenye Uwanja wa Mkwakwani. Oljoro JKT itakuwa mwenyeji wa Simba kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Sheikh Kaluta Amri Abeid jijini Arusha.
RATIBA COPA U15 KUPANGWA ALHAMISI
Ratiba ya michuano ya U15 Copa Coca-Cola ngazi ya kanda mwaka huu itapangwa keshokutwa (Agosti 29 mwaka huu) saa 5 asubuhi kwenye ofisi za Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF).
Michuano hiyo ya kanda itaanza Septemba Mosi mwaka huu wakati mikoa inakumbushwa kuwa inatakiwa iwe imewasilisha usajili wa wachezaji wao kufikia Agosti 28 mwaka huu kupitia email ya TFF ambayo nitanfootball@tff.or.tz na nakala kwa madadi_salum@ yahoo.com
Pia mikoa inakumbushwa kutowajumuisha wanafunzi wa darasa la saba katika timu zao katika ngazi ya kanda na fainali itakayochezwa Dar es Salaam kuanzia Septemba 7 mwaka huu kwa vile watakuwa katika mitihani ya kumaliza elimu ya msingi. Timu zinatakiwa kufika vituoni Agosti 30 mwaka huu.
Kanda hizo ni Mwanza itakayokuwa na timu za mikoa ya Geita, Kagera, Kigoma, Mara, Mwanza, Shinyanga, Simiyu na Tabora. Mikoa ya Arusha, Kilimanjaro, Manyara na Singida inaunda Kanda ya Arusha.
Zanzibar itakuwa na Kaskazini Pemba, Kusini Pemba na mikoa miwili ya Unguja wakati Kanda ya Dar es Salaam ina Ilala, Kinondoni, Lindi, Mtwara, Temeke na mkoa mmoja wa Unguja.
Kanda ya Mbeya inaundwa na Iringa, Katavi, Mbeya, Njombe, Rukwa na Ruvuma wakati Dodoma, Morogoro, Pwani na Tanga zinaunda Kanda ya Morogoro.
Mwanza itatoa timu nne kucheza hatua ya fainali wakati kanda nyingine za Arusha timu mbili, Zanzibar (2), Mbeya (3) na Kanda ya Morogoro itaingiza timu mbili.
Boniface Wambura
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)
EmoticonEmoticon