KAMATI KUTANGAZA MCHAKATO WA UCHAGUZI TFF LEO


Mchakato wa uchaguzi wa kamati mpya ya Utendaji ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) unatarajiwa kutangazwa hii leo (Agosti 13 mwaka huu).

Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi ya TFF, Hamidu Mbwezeleni atakutana na Waaandishi wa Habari kwenye ofisi za TFF saa 6 kamili mchana ambapo mbali ya mchakato utakavyokuwa anatarajia kutangaza tarehe mpya ya uchaguzi huo ambao awali ulitarajiwa kufanyika Septemba 29 mwaka huu.

Kamati ya Uchaguzi ya TFF ilikutana Jumapili (Agosti 11 mwaka huu) na inatarajia kuwa na kikao kingine leo (Agosti 12 mwaka huu) ambapo pamoja na mambo mengine itazungumzia maandalizi ya uchaguzi huo.

Mbali ya Mbwezeleni, wajumbe wengine wa Kamati hiyo ni Moses Karuwa (Makamu Mwenyekiti), Mohamed Sinani, Chabanga Dyamwale na Kitwana Manara.

MAGORI, LINA WAINGIA KAMATI ZA CAF

Watanzania Crescentius Magori na Lina Kessy wameteuliwa kuwa wajumbe kwenye kamati ndogondogo (standing committees) mpya za Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) zilizotangazwa juzi na Katibu Mkuu wa shirikisho hilo Hicham El Amrani.

Magori na Lina ambao ni wajumbe wa Kamati ya Utendaji ya TFF watakuwa kwenye kamati hizo kwa kipindi cha miaka miwili (2013-2015). Magori ameteuliwa kuwa mjumbe wa Kamati ya Maandalizi ya Mashindano ya Mpira wa Miguu wa Ufukweni (Beach Soccer) wakati Lina ameingia kwenye Kamati ya Maandalizi ya Mpira wa Miguu kwa Wanawake.

Makamu wa Rais wa TFF, Athuman Nyamlani ameteuliwa tena kuwemo kwenye Bodi ya Rufani ya CAF yenye wajumbe 12 kwa kipindi kingine cha miaka miwili. Nyamlani alikuwepo kwenye bodi iliyopita, na itaendelea kuwa chini ya uenyekiti wa Prosper Abega kutoka Cameroon.

Rais wa TFF, Leodegar Tenga ambaye pia ni mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya CAF yuko kwenye kamati tano za Shirikisho hilo. Kamati hizo ni Kamati ya Fedha ambayo ni Makamu Mwenyekiti na Kamati ya Maandalizi ya Fainali za Afrika kwa Wachezaji wa Ndani (CHAN).

Kamati nyingine ni Kamati ya Masoko na Televisheni ambayo ni Mwenyekiti, Kamati ya Ufundi na Maendeleo, na Kamati ya Ushauri na Vyama Wanachama wa CAF.

KAMATI YA SHERIA KUPITIA USAJILI

Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji chini ya Mwenyekiti wake Alex Mgongolwa inakutana leo jioni (Agosti 13 mwaka huu) na kesho (Agosti 14 mwaka huu) kupitia na kufanyia uamuzi usajili wa wachezaji wenye matatizo.

Hatua ya kwanza ya usajili imeshamalizika wakati hatua ya pili ya usajili inaanza kesho (Agosti 14 mwaka huu) ikihusisha wachezaji ambao watakuwa hawajasajiliwa katika Ligi Kuu ya Vodacom msimu huu na wale kutoka nje ya Tanzania.

Hivyo, dirisha la uhamisho kwa wachezaji wa kimataifa litafungwa baada ya hatua ya pili ya usajili kumalizika Agosti 29 mwaka huu.

Boniface Wambura
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)


EmoticonEmoticon