Mechi ya Ligi Kuu ya
Vodacom (VPL) kati ya Yanga na Coastal Union iliyochezwa jana (Agosti 28 mwaka
huu) katika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam imeingiza sh. 152,296,000.
Watazamaji 26,137
walikata tiketi kushuhudia mechi hiyo namba 14 ya VPL msimu wa 2013/2014
iliyomalizika kwa sare ya bao 1-1.
Viingilio katika mechi
hiyo vilikuwa sh. 5,000, sh. 8,000, sh. 15,000 na sh. 20,000 huku kila klabu
ikipata mgawo wa sh. 36,947,427.45 wakati Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT)
iliyolipwa ni sh. 23,231,593.22.
Mgawo mwingine ni
asilimia 15 ya uwanja sh. 18,786,827.52, tiketi sh. 3,818,890, gharama za mechi
sh. 11,272,096.51, Kamati ya Ligi sh. 11,272,096.51, Mfuko wa Maendeleo ya Mpira
wa Miguu (FDF) sh. 5,636,048.26 na Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es
Salaam (DRFA) sh. 4,383,593.09.
COPA COCA-COLA KANDA
KUANZA SEPT 2
Michuano ya Copa
Coca-Cola kwa vijana wenye umri chini ya miaka 15 inayoshirikisha mikoa yote ya
Tanzania Bara na Visiwani inaanza kutimua vumbi Septemba 2 mwaka huu katika
vituo sita tofauti.
Kwa mujibu wa ratiba
iliyopangwa leo (Agosti 29 mwaka huu), kituo cha Mwanza mechi zake zitachezwa
katika viwanja vya Alliance ambapo timu zitakazofungua dimba ni Kagera vs
Kigoma, Mara vs Tabora, Simiyu vs Geita na Mwanza vs Shinyanga.
Kituo cha Mbeya ambapo
mechi zitachezwa viwanja vya Iyunga ni Katavi vs Njombe, na Ruvuma vs Mbeya.
Kituo cha Pwani ni Ilala vs Kaskazini Unguja, na Lindi vs Pwani.
Ufunguzi katika kituo
cha Arusha ambapo mechi zake zitachezwa Uwanja wa Kumbukumbu ya Sheikh Kaluta
AMri Abeid ni Manyara vs Kilimanjaro, na Arusha vs Singida.
Uwanja wa Jamhuri
ambapo utatumika kwa mechi za kituo cha Morogoro, Tanga itacheza na Dodoma
wakati Morogoro itaumana na Temeke. Mjini Zanibar kwenye Uwanja wa Chuo cha
Amaan ni kati ya Kaskazini Pemba na Mjini Magharibi, na Kusini Pemba dhidi ya
Kusini Unguja.
USAILI WAGOMBEA TFF,
TPL BOARD KUANZA KESHO
Usaili kwa wanaoomba
kuteuliwa kuwa wagombea uongozi katika uchaguzi wa Shirikisho la Mpira wa Miguu
Tanzania (TFF) na ule wa Bodi wa Ligi Kuu (TPL Board) unaanza kesho (Agosti 30
mwaka huu).
Kwa mujibu wa ratiba
iliyotolewa na Kamati ya Uchaguzi ya TFF, Agosti 30 mwaka huu ni usaili kwa
waombaji uongozi wote katika Bodi ya Ligi Kuu pamoja na waombaji uongozi wa TFF
kwa kanda namba 11 (Morogoro na Pwani), kanda namba 12 (Kilimanjaro na Tanga)
na kanda namba 13 (Dar es Salaam).
Agosti 31 mwaka huu ni
kanda namba sita (Rukwa na Katavi), kanda namba saba (Mbeya na Iringa), kanda
namba nane (Njombe na Ruvuma), kanda namba tisa (Lindi na Mtwara) na kanda
namba kumi (Dodoma na Singida).
Usaili kwa kanda namba
moja (Geita na Kagera), kanda namba mbili (Mara na Mwanza), kanda namba tatu
(Simiyu na Shinyanga), kanda namba nne (Arusha na Manyara) kanda namba tano
(Kigoma na Tabora), na nafasi za Rais na Makamu wa Rais wa TFF utafanyika
Septemba Mosi mwaka huu.
Waombaji wote
wamepangiwa muda wao wa usaili. Kwa mujibu wa ratiba usaili ufanyika kuanzia
saa 3 kamili asubuhi hadi saa 2 usiku. Wasailiwa wote wanatakiwa kuzingatia
muda waliopangiwa.
Boniface Wambura
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa
Miguu Tanzania (TFF
EmoticonEmoticon