UWAKILISHI
KWENYE MKUTANO MKUU TFF
Kamati
ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ya Shirikisho la Mpira wa Miguu
Tanzania (TFF) imesema uwakilishi wa ujumbe kwenye Mkutano Mkuu
unaanzia kwenye chama cha mpira wa miguu cha mkoa, kufuatiwa na chama
shiriki na baadaye klabu ya Ligi Kuu.
Mwongozo
huo juu ya uwakilishi wa wajumbe kwenye Mkutano Mkuu umetolewa
kutokana na maombi ya Sekretarieti ya TFF kwa kamati hiyo iliyokutana
jana (Septemba 16 mwaka huu) baada ya kubaini baadhi ya wajumbe
wanashikilia nafasi mbili kwenye vyama tofauti.
Kwa
mujibu wa Ibara ya 5 ya Katiba, kuna makundi ya aina tatu ya
wanachama wanaounda TFF. Makundi hayo ni vyama vya mikoa, vyama
shiriki na klabu za Ligi Kuu.
Sekretarieti
ya TFF imebaini kuwa kuna baadhi ya viongozi wa kuchaguliwa wa mikoa
ambao pia ni viongozi wa vyama shiriki na klabu za Ligi Kuu, hivyo
wana nafasi zaidi ya moja ya kuingia kwenye Mkutano Mkuu.
Hivyo,
kutokana na mwongozo huo ushiriki wa wajumbe kwenye Mkutano Mkuu wa
TFF utaanzia chama cha mkoa, kufuatiwa na chama shiriki na baadaye
klabu za Ligi Kuu.
Pia
nafasi ambazo zinaweza kuwakilishwa kwenye Mkutano Mkuu kama mhusika
hayupo ni za Mwenyekiti atakayewakilishwa na Makamu Mwenyekiti, na
Katibu atakayewakilishwa na Katibu Msaidizi. Nafasi za
ujumbe wa Mkutano Mkuu na ile ya mwakilishi wa klabu hazina
uwakilishi kama mhusika hayupo.
LIGI
KUU YAINGIA RAUNDI YA NNE
Michuano
ya Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) kuwania ubingwa wa Tanzania Bara
inaingia raundi ya nne kesho (Septemba 18 mwaka huu) kwa mechi saba
katika viwanja saba tofauti.
Vinara
wa ligi hiyo, JKT Ruvu wanaonalewa na Kocha Mbwana Makata watakuwa
ugenini Uwanja wa Mabatini ulioko Mlandizi mkoani Pwani dhidi ya Ruvu
Shooting ya Charles Boniface Mkwasa. Mechi hiyo inatarajiwa kuwa
kivutio kikubwa kwa washabiki mkoani Pwani kutokana na aina ya soka
inayochezwa na timu hizo.
Baada
ya sare dhidi ya Mbeya City wikiendi iliyopita, Yanga inaendelea
kubaki Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine jijini Mbeya ambapo itacheza
na Tanzania Prisons katika mechi itakayochezeshwa na mwamuzi Simon
Mbelwa kutoka Pwani.
Nayo
Simba itaumana na Mgambo Shooting Stars ya Tanga katika mechi
itakayopigwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kwa viingilio vya sh.
5,000, sh. 8,000, sh. 15,000 na sh. 20,000. Mechi hiyo itakuwa chini
ya Kamishna David Lugenge kutoka Iringa.
Uwanja
wa Kaitaba mjini Bukoba utakuwa mwenyeji wa mechi kati ya Oljoro JKT
kutoka Arusha na wenyeji Kagera Sugar wakati Azam na Ashanti United
zitakwaruzana kwenye uga wa Azam Complex ulioko Chamazi jijini Dar es
Salaam.
Mwamuzi
Jacob Adongo kutoka Mara ndiye atakayechezesha mechi kati ya Coastal
Union na Rhino Rangers itakayofanyika Uwanja wa Mkwakwani jijini
Tanga. Mtibwa Sugar inarejea uwanja wake wa Manungu ulioko Turiani
mkoani Morogoro ambapo inaikaribisha Mbeya City ya Kocha Juma
Mwambusi.
Wakati
huo huo, Ligi Daraja la Kwanza (FDL) nayo inaendelea kesho (Septemba
18 mwaka huu) kwa mechi moja ambapo Lipuli ya Iringa ambayo wikiendi
iliyopita ilicheza Mkamba mkoani Morogoro inapita mjini Morogoro
kuikabili Polisi Morogoro kwenye Uwanja wa Jamhuri.
EmoticonEmoticon