Mhe. Mbashe amwomba Rais Magufuli kufanya marekebisho mazingira ya uendeshwaji Biashara


Napenda kuchukua fursa hii kwa heshima kubwa kabisa na kwa niaba ya wananchi wenzangu wa Jimbo la Nzenga Mjini kumpongeza Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Joseph Pombe Magufuli kwa uamuzi aliouchukua wa kuivunja Bodi ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na kumfuta kazi mwenyekiti wa Bodi hiyo Bw. Bernard Mchomvu, kwa kutofuata maagizo ya Mhe. Rais na matakwa ya Sheria ya Benki Kuu ya Tanzania ya mwaka 2006, kifungu cha 31 na 32 ambavyo vinaelekeza Mashirika ya Umma na Taasisi za Serikali kuweka fedha zao katika akaunti maalumu zilizopo Benki Kuu.
Uamuzi huo sio tu unawanufaisha walipa kodi wa Taifa letu lakini pia unakomesha tabia za matumizi mabaya ya madaraka na fedha za umma kwa kujitajirisha na kujinufaisha isivyo halali kwa baadhi ya Watendaji Wakuu wa Mashirika ya Umma.
Namshauri Mhe. Rais kufanya marekebisho makubwa katika mfumo mzima wa uanzishaji, uendeshaji na uratibu wa biashara nchini ili kuongeza ajira nchini, kwa kuwa ripoti ya Benki ya Dunia (2016) ya kufanya biashara Tanzania (Doing Business Tanzania- 2016) inaonesha Tanzania kutofanya vizuri katika Sera na Sheria za usajili wa biashara mpya na mazingira ya uendeshaji wa biashara kuwa kushika nafasi ya 129 kati ya nchi 189. Kwa mujibu wa ripoti hiyo mjasiriamali akitaka kuanza biashara rasmi lazima avuke vihunzi 9 ndani ya takribani siku 26 ili aweze kufungua biashara yake! Vihunzi hivyo vinavunja moyo na kupunguza kasi ya ongezeko la ajira binafsi kwa njia ya ujasiriamali na pia inalipa Taifa hasara kwa kutokusanya kodi kutoka kwenye biashara hizi mpya kwa haraka na kwa wakati kutokana na urasimu uliopo.
Pamoja na hayo pia, namshauri Mhe. Rais, agize wizara ya wiwanda na biashara na wizara ya fedha kurekebisha sheria za kodi na biashara ili kuwezesha wepesi, urahisi na uharaka wa kukusanya kodi na kuwezesha wafanyabiashara wadogo kufanya biashara kwa uhuru. Ripoti ya Doing Business Tanzania, (2016) imebainisha kuwa makampuni yanayolipa kodi huchukua saa 179 kujaza fomu za marejesho hivyo kuifanya Tanzania kuwa na utaratibu mgumu wa kulipa kodi na kushika nafasi ya 150 kati ya nchi 189 duniani kwa ugumu wa taratibu za kulipa kodi. Tukiondoa ugumu huo na kuweka wepesi, kasi ya kukusanya mapato ya kodi itaongezeka na mapato pia yataongezeka! Kwa umahususi Serikali inaweza kuanzisha kituo kimoja cha biashara kwa wafanyabiashara wadogo (one stop business center) kitakachotoa motisha kwa kuratibu uanzishaji wa biashara husika mpaka kulipa kodi kwa njia za digitali na mifumo ya TEHAMA. Vituo hivi viwepo kuanzia ngazi ya Serikali za Mitaa ili kurahisisha shughuli za uanzishaji wa Biashara na uwekezaji kutokea chini.
Marekebisho hayo ya sheria za kodi na biashara yalenge zaidi kutengeneza ‘Business Incubation’ na Misamaha ya kodi (Tax holidays) kwa wafanyabiashara wadogo wanaoanza biashara ili kusaidia kukuza biashara kuliko hali ilivyo hivi sasa ambapo biashara ndogo zinakabiliwa na mzigo mkubwa wa kodi na Tozo za ushuru mbalimbali katika halmashauri zetu kwa mfano Leseni, kodi ya huduma, kodi ya mapato, na kodi za majengo.
Pia kama taifa umewadia wakati Mhe. Rais awaagize BoT na Wizara ya Fedha katika kipindi cha miaka hii mitano ya awali kubadili ‘Modeli ya Uchumi’ wetu kutoka ‘Consumption module’ kwenda kwenye ‘Investment module’ na hii iendane na mabadiliko makubwa ya ‘Tax structure’ yetu na sheria za Uwekezaji na Biashara na kutengeneza motisha (Incentive package) za kisekta na si motisha za ya mwekezaji mmoja mmoja. Sekta muhimu ambazo zinahitaji kupewa kipaumbele kwenye hiyo new module ni sekta ya ngozi, na viwanda vya mazao ya kilimo.
Mwisho kabisa napenda kumhakikisha Mhe. Rais kuwa mimi binafsi kama mbunge, wananchi wa Jimbo la Nzega na Watanzania wengine wote tunaoamini katika uadilifu katika ofisi za umma, tunaendelea kumuombea ulinzi kwa Mungu, na tupo nyuma yake kumuunga mkono dhidi ya vita hii ngumu ya kupambana na ‘wapiga dili’ walioligeuza Taifa letu miaka 10 iliyopita kuwa shamba la bibi!


EmoticonEmoticon