WALIOKOPESHWA NYUMBA ZA SERIKALI WAPEWA MWEZI MMOJA, UJENZI WA ZINGINE 851 NAO UMEANZA


Waziri wa ujenzi nchini Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli ametoa kipindi cha mwezi mmoja kwa watumishi wa umma waliokopeshwa nyumba za serikali, kulipa madeni yao vinginevyo watanyang'anywa nyumba hizo na kupewa watumishi wengine.


Waziri Magufuli ametoa agizo hilo leo muda mfupi baada ya kuzindua ujenzi wa nyumba 851 zinazojengwa eneo la Mabwepande nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam, nyumba zitakazopokeshwa kwa watumishi wa umma.

Katika maelezo yake, waziri Magufuli amesema takribani wafanyakazi 2500 bado hawajalipa madeni wanayodaiwa, ambapo amemuomba makamu wa rais Dkt. Mohammed Gharib Bilal kuunga mkono hatua hiyo ya kutoa mwezi mmoja au kuwanyang'anya nyumba wadaiwa hao.

Wakati huohuo, makamu wa rais Dkt Mohammed Gharib Bilal, amesema muungano wa Tanganyika na Zanzibar utaendelea kudumu licha ya njama za watu wachache wanaotaka muungano huo uvunjike.
Dkt. Bilal amesema hayo leo jijini Dar es Salaam na kufafanua kuwa pasipo kujali wanatoka upande upi wa muungano, Watanzania wote ni ndugu wasioweza kutenganishwa na hila za watu wachache.

Katika suala la kuwawezesha wananchi kumiliki nyumba, Dkt. Bilal amesema kuwa serikali imepitisha sheria ijulikanayo kama “Mortgage Finance Act” ili kurahisisha upatikanaji wa mikopo yenye masharti nafuu kwa ajili ya ujenzi wa nyumba.

Hatahivyo Dkt Bilal alishauri kuwa ujenzi wa nyumba hizo usielekezwe katika miji mikubwa tu bali ielekezwe katika miji miji inayo kuwa pamoja na wilaya mpya hapa nchini ili kuongeza chachu ya maendeleo. Amesema.

Pamoja na nyumba 851 zinazo jengwa huko Bunju B, serikali itajenga nyumba zingine 1,400 katika mkoa wa Dar es salaam huku nyumba 2,510 zitajengwa katika mikoa 12 upande wa Tanzania Bara katika mwaka huu wa fedha 2013/2014.


EmoticonEmoticon