Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete
amesema kuwa Serikali yake itaongeza kwa kiasi kikubwa kasi ya
kusambaza huduma za umeme na maji vijiji kwa nia ya kuboresha maisha
ya wananchi wake
Rais
Kikwete ameyasema hayo wakati akizindua miradi ya maendeleo hii leo,
katika ziara yake ya mara ya kwanza katika mkoa mpya wa Shimiyu
ambapo mamia ya wananchi walihudhuria uzinduzi wa miradi hiyo
Rais
Kikwete ameanza ziara hiyo kwa kuweka jiwe la msingi kwenye ujenzi wa
Barabara ya Bariadi-Lamadi kwa kiwango cha lami katika sherehe
iliyofanyika katika eneo la Old Maswa katika Wilaya hiyo.
Akizindua
mradi wa usambazaji umeme vijijini katika Parokia ya Nkololo katika
Wilaya ya Bariadi, Rais Kikwete amesema kuwa katika kusambaza huduma
za umeme kwa kasi zaidi, Wakala wa Usambazaji Umeme Vijijini (REA),
utasambaza umeme katika vijiji 1,600 katika awamu ya kwanza ya kazi
hiyo katika muda mfupi.
Rais
amesema kuwa usambazaji huo wa umeme wa REA
ni tofauti na usambazaji umeme unaofanyika chini ya Miradi ya Shirika
la Maendeleo ya Milenia la Marekani na Mradi wa Electricity Five
unaogharimiwa na Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB).
Chini
ya miradi hiyo, vijiji 155 katika Mkoa wa Simiyu peke yake
vitasambaziwa umeme, kasi ambayo ilikuwa haijawahi kufikiwa wakati
wowote katika historia ya Tanzania.
Kuhusu
maji, Rais Kikwete amesema kuwa katika kipindi cha mwaka mmoja ujao,
Serikali yake inatarajia kusambaza huduma ya maji katika vijiji 1,449
katika hatua inayokadiriwa kuwa itawanufaisha watu wapatao milioni
saba.
Rais
Kikwete anaendelea na ziara yake katika Mkoa wa Simiyu kwa kutembelea
wilaya za Itilima na Meatu. Mkoa wa Simiyu ni moja ya mikoa minne
ambayo iliundwa na Rais Kikwete mwaka jana na ina wilaya tano ambazo
ni Busega, Bariadi, Maswa, Meatu na Itilima.
EmoticonEmoticon