ASHANTI UTD, SIMBA UWANJANI VPL HUKU TFF IKITAKA ORODHA YA WALIO SAMEHEWA



Mechi za kukamilisha mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) zinaanza kesho (Novemba 6 mwaka huu) ambapo Ashanti United itakuwa mwenyeji wa Simba kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.  

Viingilio katika mechi hiyo itakayochezwa kuanzia saa 10 kamili chini ya mwamuzi Andrew Shamba kutoka Pwani ni sh. 5,000, sh. 8,000, sh. 15,000 na sh. 20,000. Waamuzi wasaidizi ni Abdallah Mkomwa na Rashid Abdallah wote kutoka Pwani wakati mezani atakuwa Hamisi Chang’walu.  

Mechi nyingine za kesho ni JKT Ruvu Stars na Coastal Union (Uwanja wa Chamazi), Kagera Sugar na Mgambo Shooting (Uwanja wa Kaitaba, Bukoba) na Ruvu Shooting na Mtibwa Sugar (Uwanja wa Manungu, Morogoro).


Keshokutwa (Novemba 7 mwaka huu) raundi ya 13 kumaliza mzunguko wa kwanza itakamilika kwa mechi kati ya Yanga na Oljoro JKT kwenye Uwanja wa Taifa kwa viingilio vya sh. 5,000, sh. 8,000, sh. 15,000 na sh. 20,000.   Azam itakuwa mwenyeji wa Mbeya City kwenye Uwanja wa Chamazi wakati Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi mjini Tabora utakuwa mwenyeji wa mechi kati ya Rhino Rangers na Tanzania Prisons kutoka Mbeya.   Novemba 7 mwaka huu, Azam itacheza na Mbeya City, Yanga itacheza na Oljoro JKT kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam wakati Rhino itakuwa mwenyeji wa Tanzania Prisons.

TFF YATAKA ORODHA YA WALIOSAMEHEWA

Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limetuma waraka kwa vyama vya mpira wa miguu vya wilaya, mikoa na vyama shiriki kuvitaka kuwasilisha orodha ya wote waliofaidika na msamaha wa Oktoba 28 mwaka huu.   Oktoba 28 mwaka huu wakati akizungumza katika Mkutano Mkuu baada ya uchaguzi, Rais mpya wa TFF, Jamal Malinzi alitoa msamaha kwa wote waliofungiwa kwa sababu mbalimbali.  

Hata hivyo, msamaha huo hauwahusu waliofungiwa kutokana na makosa ya rushwa au kupanga matokeo. Vilevile haugusi adhabu zilizotolewa ndani ya klabu.   Vyama vya mikoa vinatakiwa kuhakikisha waraka huo unafika kwa wanachama wao (vyama vya mpira wa miguu vya wilaya). TFF inataka orodha ya wote waliofaidika na msamaha huo kwa ajili ya kumbukumbu zake (records).

 TANZANITE KWENDA MAPUTO KESHO 

Kikosi cha timu ya Taifa ya wanawake chini ya miaka 20 (Tanzanite) kinaagwa kesho (Novemba 6 mwaka huu) saa chache kabla ya kuanza safari ya kwenda Maputo, Msumbiji.   Hafla fupi ya kuikabidhi bendera Tanzanite itafanyika kesho saa 5 asubuhi kwenye ofisi za TFF wakati kikosi hicho kinatarajiwa kupaa saa 11 jioni kwa ndege ya LAM na kuwasili Maputo saa 3.45 usiku.

Msafara wa Tanzanite ambayo ilishinda mechi ya kwanza mabao 10-0 karibu wiki mbili zilizopita jijini Dar es Salaam utaongozwa na mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya TFF, Kidao Wilfred.   Mechi hiyo ya marudiano itachezwa Novemba 9 mwaka huu Uwanja wa Taifa wa Zimpeto, na timu itarejea nyumbani Novemba 10 mwaka huu saa 8.30 mchana kwa ndege ya LAM.   Boniface Wambura Mgoyo Kaimu Katibu Mkuu Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)


EmoticonEmoticon