JK: VIJIJI 155 KUNUFAIKA NA MRADI WA UMEME, VINGINE 1449 KUNUFAIKA NA MAJI HUKO SHIMIYU:

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amesema kuwa Serikali yake itaongeza kwa kiasi kikubwa kasi ya kusambaza huduma za umeme na maji vijiji kwa nia ya kuboresha maisha ya wananchi wake


Rais Kikwete ameyasema hayo wakati akizindua miradi ya maendeleo hii leo, katika ziara yake ya mara ya kwanza katika mkoa mpya wa Shimiyu ambapo mamia ya wananchi walihudhuria uzinduzi wa miradi hiyo

Rais Kikwete ameanza ziara hiyo kwa kuweka jiwe la msingi kwenye ujenzi wa Barabara ya Bariadi-Lamadi kwa kiwango cha lami katika sherehe iliyofanyika katika eneo la Old Maswa katika Wilaya hiyo.
Barabara hiyo yenye urefu wa kilomita 71.8 itauunganisha Mkoa wa Simiyu na mikoa ya Mwanza, Shinyanga, Mara na inajengwa na Kampuni ya China Communication Construction ya China kwa gharama ya Sh. Bilioni 67.4, fedha ambazo zinatolewa na Serikali ya Tanzania ambayo tayari imemlipa mkandarasi huyo Sh.Bilioni 21.69 na kukamilika kwa muda wa miezi 30 ijayo.

Akizindua mradi wa usambazaji umeme vijijini katika Parokia ya Nkololo katika Wilaya ya Bariadi, Rais Kikwete amesema kuwa katika kusambaza huduma za umeme kwa kasi zaidi, Wakala wa Usambazaji Umeme Vijijini (REA), utasambaza umeme katika vijiji 1,600 katika awamu ya kwanza ya kazi hiyo katika muda mfupi.

Rais amesema kuwa usambazaji huo wa umeme wa REA ni tofauti na usambazaji umeme unaofanyika chini ya Miradi ya Shirika la Maendeleo ya Milenia la Marekani na Mradi wa Electricity Five unaogharimiwa na Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB).

Chini ya miradi hiyo, vijiji 155 katika Mkoa wa Simiyu peke yake vitasambaziwa umeme, kasi ambayo ilikuwa haijawahi kufikiwa wakati wowote katika historia ya Tanzania.

Kuhusu maji, Rais Kikwete amesema kuwa katika kipindi cha mwaka mmoja ujao, Serikali yake inatarajia kusambaza huduma ya maji katika vijiji 1,449 katika hatua inayokadiriwa kuwa itawanufaisha watu wapatao milioni saba.

Rais Kikwete anaendelea na ziara yake katika Mkoa wa Simiyu kwa kutembelea wilaya za Itilima na Meatu. Mkoa wa Simiyu ni moja ya mikoa minne ambayo iliundwa na Rais Kikwete mwaka jana na ina wilaya tano ambazo ni Busega, Bariadi, Maswa, Meatu na Itilima.


EmoticonEmoticon