KAMATI ZA KUDUMU ZA BUNGE KUKUTANA MACHI 18

Kamati za Kudumu za Bunge zinatarajiwa kuanza  kukutana na kutekeleza majukumu ya Kibunge  jijini Dar es Salaam kuanzia Machi 18, ikiwa ni kipindi cha nusu muhula wa  uhai wa Bunge.
 
Vikao vya kamati hizo vitaanza mara baada ya kukamilika kwa uundwaji wa Kamati Mpya za Bunge pamoja na uchaguzi wa wenyeviti wa Kamati hizo utakaofanyika Ijumaa ya wiki hii.

Mwishoni mwa mkutano wa 10 wa Bunge mwezi uliopita, Spika wa Bunge, Anne Makinda alitangaza mabadiliko ya kamati hizo, huku akiifuta Kamati ya Hesabu za Mashirika ya Umma (POAC) iliyokuwa ikiongozwa na Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe.
 
Kutokana na mabadiliko hayo, shughuli za POAC sasa zitafanywa na Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC) ambayo itaendelea na jukumu lake la msingi la kuchambua taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) pia kwa Serikali Kuu.
 
Kamati nyingine iliyofutwa ni ile ya Sheria Ndogo, huku zikiundwa kamati mpya tatu na kuzifanyia marekebisho nyingine ikiwa ni hatua ya kuimarisha usimamizi wa Bunge kwa shughuli za Serikali.
 
Katika mchakati huo, kamati mpya zilizoundwa ni Kamati ya Bajeti, Kamati ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Kamati ya Ulinzi na Usalama ambayo imetenganishwa kutoka katika Kamati ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa.  
 
Kwa mujibu wa Spika Makinda, majukumu ya kamati mpya ya bajeti ni kufuatilia utekelezaji wa bajeti ya Serikali na sera za fedha pamoja na kuainisha na kupendekeza vyanzo vya mapato ya Serikali na kufuatilia mwenendo wa uchumi.
 
Kamati hiyo ya bajeti pia imepewa jukumu la kushauri kamati nyingine zote kuhusu bajeti.
Taarifa iliyotolewa jana na Idara ya Habari, Elimu kwa Umma na Uhusiano wa Kimataifa ya Ofisi ya Bunge iliyolenga kuufahamisha umma juu ya kuanza kwa kamati hizo nyeti za Bunge.
 
“Baada ya uundwaji wa kamati mpya na uchaguzi wa wenyeviti, litafuatia zoezi la wajumbe wapya wa Kamati hizo kuhudhuria semina maalumu kuhusu majukumu ya Kamati pamoja na kupitia mpango wa kazi (work plan)” ilisema sehemu ya taarifa hiyo.
 
Taarifa hiyo inasema ratiba iliyopo inaonyesha kuwa kamati za kisekta zitatembelea na kukagua miradi ya maendeleo iliyokasimiwa na utekelezaji wa Bajeti ya Mwaka wa Fedha 2012/13 kuanzia Machi 18 hadi Machi 23 mwaka huu.
 
“Tarehe 25 mwezi huu, Spika wa Bunge, Anne Makinda alitoa muhtasari kwa wabunge wote kuhusu mkutano wa 11 wa Bunge ikifuatiwa na kupokea Mpango wa Maendeleo kwa mwaka 2013/14 kutoka serikalini pamoja na mwongozo wa matazamio na upeo wa Bajeti ya 2013/14,” iliongeza taarifa hiyo.
 
Taarifa hiyo ilisema kuanzia  Machi 26 hadi Aprili 5, Kamati za kisekta zitafikiria na  kuchambua maombi mapya ya fedha kwa Bajeti ya Wizara zilizo chini yake kwa mwaka wa fedha 2013/14 ikifuatiwa na Serikali kufanya majumuisho kwa kuzingatia ushauri wa kamati za kisekta.Baada ya shughuli hizo za kamati, Mkutano wa 11 wa Bunge ambao ni Mkutano wa Bajeti utaanza mjini Dodoma Aprili 9.
 
“Mzunguko wa Bajeti unakusudiwa kukamilika kabla ya tarehe 30 Juni, 2013 ili kuipa Serikali muda wa kutosha kutekeleza majukumu yake,” ilibainisha taarifa hiyo.


EmoticonEmoticon