KUHUSU TOZO KWENYE
SEKTA YA TEHAMA
Katika
wiki ya pili ya Februari 2015, baadhi ya watoa huduma za mawasiliano
ya simu za mkononi walianzisha vifurushi vya mawasiliano na bei na
kusabababisha malalamiko kutoka kwa watumiaji na umma kwa ujumla.
TCRA, kwa kuzingatia upeo wa shughuli zake, imechambua hali hiyo na
inapenda kutoa maelezo na maagizo ambayo yatawezesha kuondoa
sintofahamu iliyopo na kujenga mustakabali kwa siku zijazo.
Kwa
mujibu wa Sheria ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania ya mwaka 2003,
miongoni mwa kazi za TCRA ni kufuatilia utoaji wa huduma katika
sekta inazozisimamia kwa kuzingatia kiwango cha upatikanaji wa huduma
hizo, ubora na viwango vya huduma, bei ya huduma na kuhimiza
ushindani na ufanisi wa kiuchumi. Katika kutelekeza majukumu yake,
TCRA inawajibika kupitia na kuchambua, mara kwa mara, utoaji wa
huduma katika sekta na kuchukua hatua dhidi ya chochote kinachotokea
kwenye soko, kiwe chanya au hasi.